BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA LAPASISHA AZIMIO LA UFARANSA KUHUSU BURUNDI.

12 novembre, 2015

umojaHofu ya Jumuiya ya Kimataifa ni kuona Burundi ikikumbwa na machafuko makali. Ndio maana hii leo jioni, Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lilikutana ili kupiga kura juu ya pendekezo la Ufaransa lenye dhamira ya kuwawekea vikwazo wale wote wanaochochea vurugu na hata kulazimu mazungumzo kati ya wadau wote nchini Burundi ili hatimae kupata suluhu ya kudumu na itakayokubaliwa na pande zote.

Hii leo alkhamisi ya Novemba 12 mwaka 2015, Umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, wametoa tangazo la pamoja linalowataka serikali na Upinzani kukutana haraka sana ili kusitisha vurugu na kupatishia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa sasa.

Viongozi waandamizi wa jumuiya hizo, walitoa wito huo huko visiwani Malta walipokutana ili kujadili mfumo wa kuhimili wimbi la wakimbizi kutoka Afrika na wanaoelekea barani Ulaya na hivo kusababisha vifo vya mamia ya watu wanaokufa maji wakijaribu kuvuka na kuingia kwenye ardhi ya ulaya.

Msimamo ni ule ule, mazungumzo hayo ni lazima yaendeshwe mjini Kampala Uganda ama Addis Abeba, Ethiopia na yasimamiwe na Yoweri Museveni, msuluhishi alieteuliwa na Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki tangu mwezi Julai mwaka huu.

Katika zoezi hilo la kura hii leo katika baraza la usalama la umoja wa mataifa, kuna uwezekano, endapo serikali itaendelea kukaidi, kutumwa kwa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa na hata vile vya umoja wa afrika. Hata hivyo, Katibu mkuu wa umoja wa mataifa anazo wiki 2 ili kusahihisha hilo.

Kwa mujibu wa kifungo nambari 7 , umoja wa mataifa unaruhusiwa kutumia nguvu ili kurejesha amani. Hilo ni lazima liafikiwe na tume maalum ya umoja wa mataifa ama likubaliwe na nchi husika.  Tayari kwa pamoja, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha Azimio lilotolewa na Ufaransa.

Wengi walikuwa wakihofia uzito wa kufaanikisha hili, kutokana na Urusi, ambayo ina kura ya turufu yaani « droit de Veto » katika baraza hilo la umoja wa mataifa, kupinga vikali kwa muda kadhaa azimio hilo na kutaja kuwa, hayo ni matatizo ya ndani ya Burundi yanayotakiwa kusuluhishwa na warundi wenyewe. Hata hivyo, katika kura ya hii leo, NCHI ZOTE ZIMEAFIKI AZIMIO HILO.Hata hivyo, serikali ya Bujumbura, kupitia mshauri wa rais anaehusika na mawasiliano, Willy Nyamitwe, imekwishataja wazi kuwa inapinga vikali azimio hilo na kutaja kuwa kamwe hawawezi kulazimishwa sehemu inayotakiwa kuendeshwa mkutano huo.
Baadhi ya wanadiplomasia wanahofia pia uingiliaji kati wa rais Paul Kagame wa Rwanda, baada ya kuwatuhumu viongozi wa Burundi kuwa wanawaua kiholela raia wao usiku na mchana. Uhusiano baina ya nchi mbili hizo jirani ni mbaya mno na wote wanatupiana lawama na tuhma mbalimbali.

Bila shaka kuna hatari ya kuzuka machafuko mabaya nchini Burundi, lakini mpaka muda huu, hakuna sababu zozote zinazoweza kubaini kuwa, kuna mpango wa mauaji ya kimbari unaowavizia watutsi pekee. Jambo la muhimu, ni kuepuka kukuwa kwa vurugu na mauaji na wadau wote wakubaliane ili hatimae mgogoro huu umalizike.

Marekani nayo inaendelea kuvalia njuga tatizo la Burundi. Baada ya Mjumbe wa Rais Obama kumaliza ziara yake ya siku mbili mjini Bujumbura, sasa, Bwana Thomas Perriello amejielekeza nchini Uganda ili kuzungumza na rais wa nchi hiyo, na kumtaka aitishe mkutano wa haraka baina ya serikali na Upinzani.

Pia, Rais wa Marekani mwenyewe aliongea kwa simu na yule wa Afrika ya Kusini. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, hiyo jana, rais wa marekani Barack Obama, aliongea kwa njia ya simu na rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma ili kumuelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Burundi.

Rais Obama amemuomba Rais Zuma kuendelea kushirikiana na watendaji wengine wa kikanda ili kutoa wito wa utulivu na kuhamasisha mjadala ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa sasa.

Watu zaidi ya 200 wameuwawa na wengile laki mbili kuihama nchi tangu mwezi April, pale Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kugombea muhula wa tatu ambao kwa mujibu wa wapinzani, unakiuka katiba na mkataba wa Arusha.

Jumuiya ya kimataifa inahofia kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kama hapo awali, vilivyosababisha vifo vya watu laki tatu.

BAKARI Ubena

MGOGORO NCHINI BURUNDI WAELEKEA KUWA SUGU NA MAUAJI YAKITHIRI.

8 novembre, 2015

bjMauji hayo ya kinyama yaliendeshwa hiyo jana jumamosi majira ya saa mbili usiku katika mgahawa maarufu kama
 » Au coin des amis » tarafani Kanyosha mjini Bujumbura.

Wavamizi waliwalazimisha watu wote kuingia ndani na kuwalaza chini na ndipo kuanza kuwatuhumu kuwa wanazo silaha wanazotakiwa kuzirejesha.

Kabla hata ya kupata fursa ya kujitetea, walivurumishiwa mvua za risase na ndipo watu saba kufariki papo hapo na wengine 2 kujeruhiwa vibaya na kuwahishwa hospitali kwa matibabu. Nao, wameiaga dunia asubuhi ya leo kutokana na majeraha yao makali.

Mauaji hayo yanatokea siku ya mwisho iliyotolewa na serikali kwa raia walio na silaha kuzisalimisha kwa vyombo vya dola na la sivyo, polisi wachukue hatua kali dhidi yao za kuwapokonya.

Mauji hayo yanatokea pia siku moja kabla ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kukutana ili kujadili swala la Burundi. Pia, itazingatiwa kuwa mfanyakazi wa shirika la PNUD ni miongoni mwa waliouwawa.

Kwa mujibu wa shuhuda aliesalimika katika tukio hilo baada ya kufyatuliwa risase la kiunoni, ametaja kuwa, majambazi hao walijihami kwa silaha nzitonzito na walikuwa wakivalia sare za polisi. Gari walilopora na kuendesha unyama wao huo, ilikutwa tarafani Kanyosha asubuhi ya leo ikiwa imeharibishwa na cheche za gruneti.

Meya wa mji wa Bujumbura, Freddy Mbonimpa, amelaani tukio hilo na kuliita la kinyama sana.

Kwa siku kadhaa sasa, wakaazi wa tarafa zenye upinzani mkali kwa serikali ya sasa, wameanza kuyahama makaazi yao wakihofia kumaliziwa maisha.

Watu wengine watatu kutoka familia moja (Baba, Mama na Mtoto) waliuawawa kwa kuvurumishiwa gruneti usiku wa ijumaa hii kuamkia jumamosi huko katika kijiji cha Rugoma wilayani Kinyinya mkoani Ruyigi mashariki mwa Burundi. Wahusika wa unyama huo hawajafahamika wala hawajakamatwa.

Watu zaidi ya 200 wamekwishauwawa na wengine laki mbili kuihama nchi tangu mwezi april mwaka huu, pale Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kugombea muhula wa tatu ulio kinyume na katiba ya Burundi na hata mkataba wa amani na makubaliano wa Arusha uliosainiwa mwaka 2000 na kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi vilivyodumu kwa takriban miaka 20 na kusababisha maelfu ya vifo vya raia.

BAKARI Ubena

SHINIKIZO LA JUMUIYA YA KIMATAIFA KWA BURUNDI LAENDELEA.

6 novembre, 2015

Katika tangazo la baraza la amani na usalama la Umoja wa Mataifa la oktoba 17, walitoa wito kwa serikali ya Burundi kuanzisha mazungumzo na upinzani mjini Kampala ao Addis Abbeba, yatakaowajumuisha wahusika wote. Wito huo, uliungwa mkono na Umoja wa Ulaya, Marekani na hata Umoja wa Mataifa.

Ili kujibu wito huo,serikali ya Burundi iliteua tume ya taifa ili kuendesha mazungumzo baina ya warundi, CNDI kifupi chake kwa kifaransa na yenye muhula wa miezi 6. Mazungumzo hayo bila shaka, yatawatenga wapinzani wanaodaiwa kuwa waliendesha jaribio la mapinduzi, na ambao wanasakwa na vyombo vya sheria nchini Burundi.

Kwa upande wa serikali, wanadai kuwa, yatakuwa mazungumzo ya kitaifa baina ya warundi bila ya kuwepo upatanishi wa kimataifa. Na hivo, tume hiyo itashughulikia matatizo kadhaa yaliyotokana na uchaguzi uliopita na hata kutafutia suluhu mgogoro wa kiusalama na hata ule wa kisiasa.

Hata hivyo, tume hiyo ya CNDI bila shaka haiaminiki na haina uzito wowote mbele ya jumuiya ya kimataifa na tayari wameonyesha kuwa hiyo si suluhisho kwa mgogoro wa sasa, kwa kuwa, wanaepuka kuendesha mazungumzo ya kina na wapinzani wote.

Kwa mujibu wa taarifa kuhusu Burundi ya msemaji wa Muwakilishi na Makamo rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, iliyotolewa hii leo ijumaa, Novemba 6, Kuendelea kwa vurugu nchini Burundi ni ishara kuwa mgogoro wa sasa unapevuka.

Kauli za hivi karibuni za viongozi wa serikali zinaweza kuchochea hali ya sasa na ndio maana Umoja wa Ulaya unawatolea wito wadau wote kujizuia na kuheshimu majukumu yao. Kuchochea ghasia na mgawanyiko ni tishio kubwa na la ziada kwa usalama na utulivu wa nchi ya Burundi.

Umoja wa Ulaya umeendelea kuwaonya viongozi wa serikali kushiriki katika mashauriano chini ya ibara ya 96 ya Mkataba wa Cotonou ili kupatia ufumbuzi utakaokubalika na pande zote ili kukomesha ukiukwaji wa vipengee muhimu vya haki za Binaadamu ambazo ni kanuni za kidemokrasia na utawala bora.

Mashauriano hayo ambayo yataendeshwa kwa nia ya majadiliano na ushirikiano, yatakua pia na lengo kuu la kuunga mkono juhudi za kuhakikisha amani ya kudumu nchini Burundi.

Umoja wa ulaya umepongeza na kuunga mkono kauli ya mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika ya novemba 4, na kutaja kuwa itatoa msaada wake kunako juhudi za upatanishi wa Uganda na hata ule wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki.

Hatimae, umoja wa ulaya kupitia muwakilishi wake mkuu, wanataraji kuwa Serikali ya Burundi itatumia kila liwezekanalo ili kuanzisha mazungumzo ya kitaifa kwa kuheshimisha mkataba wa amani wa Arusha.

BAKARI Ubena

MABADILIKO YA HALI YA HEWA NI TISHIO KUBWA KWA ULIMWENGU…

3 novembre, 2015

rcUhaba wa maliasili, watu kuyahama makaazi yao na sera mbovu za maendeleo, haya ni baadhi ya matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaathiri mno sekta ya kilimo na ufugaji, nishati, afya na hata mazingira.

Wataalam wanashauri kuwa, mjadala wa umma ni lazima ufanyike kati ya viongozi wa serikali na wale wa vyama vya kiraia na lengo ikiwa ni kubuni mikakati ya kukabiliana na mabadiliko hayo.

Mtazamo wa maprofesa wa jiografia unataja kuwa, binaadamu ndie sababu kuu na ya moja kwa moja ya ongezeko la joto duniani. Na hii husababishwa na shinikizo la idadi ya watu.

Mfano nchini Burundi, kwa muda wa miaka 30 iliyopita, idadi ya watu imeongezeka maradufu na kutoka milioni 3 mpaka 10 kwa katika eneo moja.

Mbaya zaidi, idadi hii ni asilimia 90 ya watu wa vijijini wanaoishi kwa kutegemea maliasili. Na hii ni pigo kubwa kwa misitu, ardhi na kadhalika. Ndio maana kumependekezwa upandaji miti, ujenzi wa hifadhi ya maji kwa ajili ya umwagiliaji kilimo, matumizi yenye busara kwa ardhi na kupunguza shinikizo la idadi ya watu.

Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi tayari yameanza kujionyesha nchini Burundi na kusababisha mafuriko sehemu kadha. Ni muda muafaka wa kuanzisha ushirikiano wa umma ili kupambana na hali hiyo. Zaidi sana, raia waelimishwe ili kuheshimu na kuboresha mazingira wanayoishi.

Itafahamika kuwa, Mkutano wa umoja wa mataifa utakaovijumuisha vyama vilivyo chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, utafanyika nchini Ufaransa disemba mwaka huu.

BAKARI Ubena.

MSIMAMO WA CNARED BADO HAUJABADILIKA.

23 octobre, 2015

Screenshot_2015-10-23-23-11-09-1Msemaji wa Tume ya kitaifa CNARED, Chauvineau Mugwengezo ametaja kuwa, msimamo wao bado upo palepale. Bado wanaupinga uchaguzi uliopita nchini Burundi na hata muhula wa tatu wa Pierre Nkurunziza ulio kinyume na mkataba wa Arusha. Kuhusu majadiliano yanayotarajiwa mjini Kampala, ametaja kuwa, hayo ndio yatakuwa pia kiini cha malalamiko yao.

Bwana Mugwengezo alitaja pia kuwa, hawaitambui tume ya majadiliano baina ya warundi iliyoundwa na serikali ya sasa eti kwa kuwa, haiwajumuishi wapinzani wanaotambulika nchini Burundi na wenye dhamira ya kuwatetea wananchi.

Amemalizia kwa kutaja kuwa, Pierre Nkurunziza na kundi lake, hawana budi kukubaliana na hali halisi na hatua zitakazochukuliwa kunako mazungumzo hayo eti kwa kuwa, pengo alilonalo kwa sasa, litazidi kuwa kikwazo kwake endapo ataendelea kukaidi na kutaka kutawala kimabavu.

Hata hivyo, ametaja kuwa,dhamira nyegine kuu ya CNARED ni kurejewa kwa uchaguzi mkuu nchini Burundi, ili hatimae wananchi waweze kuchagua taasisi bora za nchi ambazo zitatembelea misingi ya utawala bora bila ya kumtenga yeyote.

Ukitaka kusikiliza mahojiano ya Chauvineau MUGWENGEZO alipokuwa akihojiwa na BAKARI Ubena, tembelea tovuti ya : www.indundi.com/makala

KIPINDI: LADHA ZA KWETU: 17.10.2015

17 octobre, 2015

BAKARI Ubena./2015

KIPINDI: JAMVI LA HUBA: 15.09.2015.

15 octobre, 2015

BAKARI Ubena./2015

MAKALA: 12.10.2015:USIKU

12 octobre, 2015

UKITAKA KUYAPATA MAKALA KWA KILA SIKU, TEMBELEA TOVUTI YA: www.indundi.com/makala

BAKARI Ubena./2015

PATA MAKALA KUPITIA: INDUNDI.COM

3 octobre, 2015

Habari zenu wapendwa, Natumaini hamjambo popote pale mlipo na hii ndio furaha yangu. Nipende kuwafahamisha kuwa, MAKALA yanapatikana pia kwenye mtandao wa : www.indundi.com/makala

BAKARI Ubena./2015Screenshot_2015-10-03-10-41-36-1

MAKALA: 29.09.2015: JIONI (1).

29 septembre, 2015

B.Ubena

1234