Archive pour juin, 2012

MIAKA 50 YA UHURU WA BURUNDI .

14 juin, 2012

Hymne national du Burundi sur \ »Youtube\ » MIAKA  50 YA UHURU WA BURUNDI . dans Liens bdi-flag

Nitangulize salamu zangu za dhati kwa wasomaji wangu wapendwa, pia nikichukua fursa hii kukutakeni radhi kutokana na ukimya wa muda kadhaa bila ya kukutana nanyi kunako makala kama hizi.

Hakika, kila sifa njema anastahili apewe Mola wa viumbe wote, alieweza kuumba usiku na mchana, akaumba ardhi na mbingu bila ya kuweka nguzo. Tumuombe Maanani atuongoze tuwe miongoni mwa waja wake wema, atupatie maisha marefu yenye furaha, usalama na amani hapa duniani mpaka huko mbinguni.

Atuongoze pia tuwe ni wenye kumkumbuka kila wakati, atuwezeshe kuishi kwa kupendana na kuhurumiana, tuachane na kufanyiana hiyana na atufanye ni wenye kusaidizana. Pia, asituweke kuwa ni wenye huzuni wakati wote na atuondolee shida zetu za utafutaji wa riziki zinazotutesa kila wakati. (Amin)-

Kama kinavoashiria kichwa cha habari, nchi yetu Burundi inajiandaa July mosi mwaka huu wa 2012, kusherehekea sikukuu ya miaka 50 ya Uhuru wake kutoka kwa wakoloni « Ubelgiji ».

Wengi miongi mwetu, tunaiona siku hiyo ya kipekee kama tuu sherehe ambapo wafanyakazi na wanafunzi, jeshi na polisi hufanya gwaride mbele ya rais wa jamhuri huku harakati mbali mbali za kunogesha sherehe hiyo zikiendelea kutuburudisha.

Sintothubutu kuwalaumu wenzangu wanaofanya hivo, lakini binafsi, huwa napendelea kusherehekea kitu ambacho kwa dhati moyoni kinanifurahisha ao japo kinachonipa sababu kadhaa za kufanya hivo. Hapa, nang’amua kwamba, ni busara zaidi kutatmini kwa makini ni yapi mafaanikio ambayo nchi yetu imeyafikia katika kipindi chote hicho cha miaka 50 hadi sasa.

Sintoweza kuchambua vipengee vyote muhimu ambayo nchi yoyote duniani huwa inajaribu kuviboresha ili kujiona kufikia maendeleo inayotarajia. Hebu nijikite kwa mambo mawili tu (2) muhimu ambayo Burundi inahitaji kuendeleza kujiimarisha zaidi.

  1. KUSIKILIZANA na KUVUMILIANA KATIKA HOJA:

Sote tunafahamu kuwa nchi yetu imekwisha kumbwa kwa maraa kadha na machafuko mengi na yenye sababu mbalimbali ambazo sintopendelea kukumbushia kwa leo. Na hii hutokana haswa na tatizo la kutokuwa na ukomavu wa kisiasa kwa kutosikilizana na kuvumiliana katika hoja.

Sifa moja kubwa ya mwanademokrasia popote duniani, ni kukubali kusikiliza mawazo tofauti na yale aliyonayo yeye. Kinyume na hapo, mtu huyo huchukuliwa kama ‘dikteta’.

Unapotoa fursa ua kusikiliza, bila shaka utakuwa na nafasi ya kuyatafakari na kuyachuja mawazo ya mwenzio, lakini ukikataa kutoa fursa ya kusikiliza basi utaendelea kuwa na mawazo ya aina moja tuu. Yaani yale yanakufurahisha na ambayo kwa vyovyote yatakuwa hayajengi zaidi ya kubomoa.

Kwa hili pekee, serikali yetu ya sasa inayoongozwa na rais Pierre NKURUNZIZA, ina sifa mbaya mno hadi kimataifa inatambulika. Huwa hawatoi fursa kwa mtu mwengine alie na mawazo tofauti na ya kwao, kujenga hoja yake, kwao mtu huyo ni adui mkubwa na anaweza kujikuta katika mazingira ya hatari sana.

Ni mara ngapi watu wamefungwa bila hatia, wengine kuendeshea vipigo na mateso ya kinyama, wengine kulazimika kuihama nchi yao na baadhi kulazimika kukaa kimya kwa hofu ya uhai wao.

Watetezi wa haki za binaadamu, wanahabari, wanasiasa wa upinzani, raia wa kawaida, wanaendelea kuyapata matatizo makubwa nchini Burundi kutokana tuu na fikra ao hoja yao (japo nzuri kiasi gani) ambayo ipo kinyume na serikali ya sasa.

Kukubali kusikiliza hoja ya mwengine, haimaanishi kukubaliana na kile unachokisikiliza, lakini ile tuu kutoa fursa ya kusikiliza mawazo tofauti kunaweza kutoa fursa kwako kutumia hoja zilezile alizokuwa akizitoa yule ulieamua kumsikiliza na kujenga hoja mpya na hatimae kumuaminisha mtu yule.

Ni jambo la kusikitisha mno kwa wanasiasa wa Burundi kuwa na moyo mdogo sana wa kuvumilia mawazo tofauti na ya kwao na kukosa sifa hii ya kuwa wanademokrasia. Na hili halijaanza katika awamu hii ya Cndd Fdd, bali ni tangu kitambo, na kama nilivofahamisha hapo mwanzoni, ndio kiini cha mapigano yaliyotokea na yatakayoweza kutokea (Mola atuepushe kwayo) iwapo hili halitozingatiwa.

Ni jambo la kawaida watu kutofautiana kimtazamo na kimawazo, kwa kuwa si rahisi warundi wote, hasa wa karne hii, sote tukawa wafuasi wa chama fulani cha siasa hata kama kingelikuwa kimoja, lazima wengine watakuwa na mawazo mbadala. Hii ni kwa kuwa kila mtu anayo haki ya kuamini katika kile anachopendezwa nachona hapaswikuhukumiwa ama kuonekana ni msaliti kwa kuwa tu haungani au hakubaliani na kile kinachoaminiwa na kundi lingine la watu.

Na hili linapaswa kuwapo hata kwa viongozi na wasio viongozi. Wajue kuwa mawazo yao sio sahihi daima na anapotokea mtu akawakosoa, basi wawe tayari kusikiliza na kujirekebisha kama watagundua uzito wa hoja itakayotolewa.

Kwa kufanya hivi, tutafikia jambo hili jema na kuamini kwamba: ‘SIASA SAFI NI ILE AMBAYO VIONGOZI WANAKUBALI KUKOSOLEWA’ pale wanapokwenda tofauti na matarajio ya wengi na hapo bila shaka nchi yetu itakaa katika amani na utulivu wa kudumu, ambayo ni dhamira ya kila mwananchi alie ndani ao nje ya Burundi.

  1. BURUNDI, NCHI ‘OMBA OMBA’ DUNIANI:

Ni wazi kwamba Burundi ni miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kwa kupewa misaada kutoka wahisani mbalimbali. Wahisani wakubwa kwa mipango ya maendeleo kwa nchi yetu ni Umoja wa Ulaya, Benki ya maendeleo ya afrika, Benki ya dunia na shirika la fedha duniani.

Cha kushangaza ni kuwa kulikoni Burundi imepokea misaada mingi kiasi hichotangu ipate Uhuru, lakini imebaki kuwa moja kati ya nchi ambazo wananchi wake wanaogelea katika umaskini wa kutisha, kiasi cha wengi kuishi chini ya dola moja kwa siku.

Jibu kwa mshangao huo ni kwamba, nchi haiwezi kusonga mbele kimaendeleo kutokana na utegemezi mkubwa wa misaada hiyo ya wahisani na haswa matumizi yake mabaya ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa Utawala Bora ambapo asilimia kubwa ya misaada hiyo ikimezwa na vitendo vya rushwa. Mfano hai na wa hivi karibuni, kesi inayoshakiwa kuwa ya rushwa inayoendelea nchini Ubelgiji ambayo mhusika mkuu ni Ombusman wa Burundi, Muhamed RUKARA. Mtu ambae angetakiwa kuwa msuluhishi wa taifa na mwenye kutoa mfano mwema.

Ni aibu iliyo je kwa viongozi wetu kuwa na tabia chafu kama hizi kwa kukosa uzalendo na hata chembe ya huruma kwa kiwango kikubwa cha wananchi ambao wanaendelea kuishi maisha duni kwa ukosefu wa nyanja bora za elimu, uhaba wa miundombinu (hospitali, barabara,makaazi,katika kilimo,…), afya bora, maji safi, na kadhalika.

Sote kwa pamoja, tunapaswa kuamka na kushikamana kwa kuilazimisha serikali kuwashtaki watuhumiwa wote wa kashfa za rushwa, na adhabu kali zitolewe kwa watakaobainika kisheria. La sivyo, watazidi kunufaika watu wachache na nchi kuendelea kuwa maskini.

Kiongozi mwema ni yule ambae anae wajali wale anaowaongoza, kwa kufanya kila aliwezalo waishi katika hali ya utulivu wa nafsi, haswa kwa kuweza kukidhi mahitaji yao muhimu ya kila siku. Nayo ni kupata chakula, mavazi na makaazi. Pia, kuboresha maisha yao katika mambo mengine yeliyo muhimu kama usalama, elimu, afya, michezo na kadhalika.

Si maanishi kuwa, ni jambo rahisi ama liwezalo kutekelezwa kwa muda mfinyu, lakini endapo tukiwa na uzalendo wa kutosha, kwa kutumia ipasavyo pesa ya wananchi kwa ajili yao, hilo linawezekana. Tusisahau kuwa « Penye nia kuna njia ».

Hatimae, tuwa WAZALENDO, WAVUMILIVU na haswa WAKOMAVU katika dhamira ya kuiendeleza nchi yetu. Kwa kuwa hata siku moja, haki ya mtu huwa haipotei bali hucheleweshwa tuu. Na mafaanikio siku zote hutokana na kuwa na uvumilivu na subira hata kama unaona kitu chako si kizuri, huna sababu ya kukitupa. Unachopaswa ni kuangalia namna ya kukiboresha ili kipendeze.

BURUNDI, nchi yetu ya « maziwa na asali », daima tutakulinda na kukupenda!

« Haki zote zimehifadhiwa »

Imeandikwa mjini Brussels, Juni 14, 2012

na : BAKARI Ubena.-

 » Salaamu zangu za dhati kwa warundi wenzagu popote walipo bila ya kuwasahau wagonjwa wote, wafungwa ( haswa kwa mwanahabari mwenza: Hassan RUVAKUKI, mwanasiasa: El Hadj Hussein Radjabu), marais wote walioiongoza nchi yetu, na hata wa sasa Pierre Nkurunziza, nikiwaombea wepesi katika majukumu hayo makubwa.  »