Archive pour juillet, 2012

KONGAMANO LA KWANZA LA KIHISTORIA KWA WASWAHILI WA BURUNDI.

23 juillet, 2012

KONGAMANO LA KWANZA LA KIHISTORIA KWA WASWAHILI WA BURUNDI. dans Liens conferHabari wasomaji wangu wapendwa. Ni furaha isiyo kifani kukutana nanyi tena kunako safu hii. Nimshukuru Mola kwa kuendelea kuniazima pumzi na afya njema hadi kufkia utekelezaji wa hili na mengineyo mengi yanayogubika maisha yangu ya kila siku, pia nizidi kumshukuru kwa Kuendelea kunijaalia mema na kuniepusha na mabalaa. Kwa niaba yenu sote, namuomba Atusamehe, Atuongoze na Atupe mwisho uliyo mwema. (Amin).

Kwa mara ya kwanza kabisa, kulihudhuriwa kongamano la kwanza kabisa na ambalo ni la kihistoria kwa waswahili wa Burundi. Kongamano hilo liliendeshwa mjini Brussels Ijumaa ya tarehe 13 Julai 2012, kwa kuandaliwa na Jumuiya ya Waswahili  » JUWA », shirikisho la kitamaduni. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi mdogo upatikanao Schaerbeek (Place de la Reine 12).

Licha ya kuanza kwa kuchelewa takriban dakika thelathini (30) ili kuendelea kuwasubiri washiriki wa kongamano lenyewe, bado idadi ya watu waliohudhuria ilikuwa si ya kuridhisha mno hadi kudhihirika kuwa asilimia kubwa ya viti kubaki vitupu. Ila binafsi, hilo si tatizo, maana, bora jiwe la dhahabu kuliko mlima wa tope.

Mkutano ulifunguliwa kwa riwaya ndogo ya Sheikh Salum Issa kwa utangulizi na kumpa fursa Ahmadi Kassa kuanza rasmi kuelezea sababu na umuhimu wa kongamano lenyewe na kufahamisha kuwa Ubelgiji imechaguliwa kuupokea mkutano huo wa kwanza kutokana na sababu kadhaa za kihistoria.

A.Kassa alifahamisha ya kwamba, haitoshi kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Burundi kwa sherehe pekee bali pia kutumia fursa hiyo kuyatafakari mengi baina ya maswali yanayoikabili jamii yetu, kama vile kuifahamu historia ya waswahili wa Burundi na ni upi mchango wa waswahili katika kugombea uhuru wa nchi hiyo.

Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya Mwanahistoria na Professa Christine DESLAURIER, ambae pia alikuwa mgeni rasmi, kuyaweka bayana maswali hayo ambapo aliyafafanua kwa takriban masaa mawili huku watu wakionekana kunogewa na kutaka asimalize kuongea. Lakini, kabla kabisa hajaanza kusimulia historia hiyo tamu, alifahamisha ya kwamba kuna uwezekano kwa anaehitaji kupata historia zaidi ya Burundi kabla na baada ya Uhuru, kuzitembelea Ofisi za Idara ya « Kumbukumbu » za Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji zipatikanazo mjini brussels. Kwa kuwa, baada ya miaka 50, sheria zimebadilika na kuna nyaraka ambazo zimewekwa wazi kwa wasomaji tofauti na hapo awali.

Hapo alisisitizia kuhusu waraka nambari { BUR ,64} katika kumbukumbu, unaoweka wazi ya kwamba, si pekee chama UPRONA kilichosimama kidete kwa kupigania UHURU wa BURUNDI, bali hata kabla yake kulikuwepo chama UNARU pia hata na raia kadhaa wazalendo waliojaribu kusitisha Ukoloni kwa njia moja ama nyengine. Mfano wao ni INAMUJANDI alieitwa mchawi kwa kupambana moja kwa moja na wawakilishi wa wakoloni. WAKULIMA ambao walitumia mfumo wa kukojolea mimea ya kahawa waliopanda ili kuhujumu amri za ukoloni, na kadhalika.

Baaada ya kufahamisha ni jinsi gani shirika-chati za Ukoloni zilivokuwa, bi Christine aligusia swala nyeti na kuonyesha ni kwa nini WASWAHILI walinyanyaswa na hata kutengwa na Wakoloni wa Ubelgiji ili wasipate elimu na mengineyo. Sababu kuu ilikuwa ni kutokana na dini yao. Ikiwa Ukoloni ni wa Kikristo na asilimia kubwa ya waswahili ni waislamu, basi wakoloni hao walifanya kila njama ili kuhujumu jamii ya waswahi na hata wa protestanti. Katika kipindi hicho, Buyenzi ilikuwa na idadi ya raia elfu kumi (10.000) na kwa mujibu wa wakoloni, pasenti sitini (60%) ni wakongomani, pasenti thelathini (30%) warundi na pasenti zengine nane (8%) ni wanyarwanda, wakati ambapo raia wote hao, kwa ukweli na kisheria walikuwa ni warundi. Inafahamika wazi ya kwamba, raia hao walikuwa na uhusiano wa karibu na Tanganyika ( ambayo ni Tanzania kwa sasa). Na waswahili wengi walipatikana katika maeneo ya BUYENZI, BWIZA, RUMONGE, NYANZA-LAC na KITEGA (kwa sasa GITEGA).

Kutokana na utafiti mpana na kwa mtazamo wake, Professa Christine anamnadi « SALUM HASSAN MASHANGWA » kama shujaa wa utetezi wa Uhuru wa Burundi, kuanzia miaka ya 1956. Licha ya kuwa na chimbuko la Tanganyika, alikuwa mtu muhimu katika chama UNARU, pia mfadhili. Alimiliki magari kadhaa, alifaanikiwa kuunda Ofisi binafsi ya Uchapishaji (MURASABE, UHURU na UMOJA) ambazo zilikuwa zikizagazwa kwa siri, kwa kuhofia wakoloni. Pia, mnamo miaka hiyohiyo ya 1956, aliunda chama cha kitamaduni « BARAFU NYEUPE », ambacho kiliwakusanya asilimia kubwa ya akina mama na yeye kushikilia nyadhifa ya Katibu mkuu, kwa kuwa kipindi hicho, ilikuwa hairuhusiwi kuunda chama cha kisiasa. S.H.MASHANGWA, alitumia ujanja kwa kuwasajili akina mama wengi katika chama chake, ili waweze kuzagaza nakala zake hadi Tanganyika, kwa kuwa wao walikuwa hawatiliwi sana mashaka wala kukaguliwa sana mipakani tofauti na wanamume.

Pia, mnanzoni mwa mwaka 1958, MASHANGWA akishirikiana na wengine kama akina BICHUKA, walimuunganisha Mwanamfalme Louis RWAGASORE na Rais wa TANGANYIKA, J.K. NYERERE, alipotuwa kwa muda mjini USUMBURA akielekea GHANA katika Mkutano mkuu wa ACCRA wa march 1958). Ni baada ya hapo, mnamo mwaka 1959, ndipo kukaruhusiwa uundwaji wa vyama vya kisiasa na moja kwa moja kukaundwa chama UNARU, baadae UPRONA na vinginevyo. Mwanzoni, licha ya kuwa na upinzani mdogo, vyama hivyo viwili, vilikuwa na dhamira moja, ambayo ni kugombea UHURU WA BURUNDI.

Waliyohudhuria kongamano hilo, watakubaliana nami ya kuwa, historia hiyo ya kabla, wakati na baada ya uhuru, ni ndefu mno, kama alivotaja mwenyewe Prof.Christine. Picha za sanamu (video) zilizochukuliwa siku hiyo pia na usomaji wa vitabu, ndio utawasaidia kuyafahamu mengi zaidi. Binafsi, nilifurahishwa na alivodadisi swala nzima la kihistoria na kuonyesha umuhimu wa waswahili katika kupambana na kupigania uhuru wa Burundi.

Kabla ya kumalizika kongamano hilo, alipewa nafasi mwanaharakati mkubwa wa swala zima la waswahili wa Burundi, Abdoul MTOKA ambae pia ni mwanasheria, aliefafanua kwa mukhtasari sababuza kupigania Uhuru na kusisitiza kuhusu Unyanyasaji waliofanyiwa waswahili nchini Burundi, hali ambayo bado inaendelea hadi sasa. aliweka wazi kwamba, watu huwa hawagombei uhuru ili wasitishe pekee ukoloni, bali pia waweze kupata mafaanikio ya uhuru wao ambayo yalikuwa yakizuiliwa na Ukoloni.

Na moja wapo mwa hayo ni: – Kutengwa katika utapataji wa elimu

- Kulazimishwa kulipa kodi na ushuru vya hali ya juu

- Kufurushwa kinyume cha sheria katika makaazi yao  (ardhi zao) bila ya kupewa viinua mgongo, nk.

Na hadi sasa, twaadhimisha miaka 50 ya Uhuru, na nina imani kwamba bado kuna unyanyasaji kwa waswahili wa Burundi na kazi kubwa bado inahitajika kufanyika ili kufikia malengo thabiti. Pia, A.MTOKA, aligusia kuhusu historia ya waswahili ili kuonyesha wazi kwamba si wageni la wahamiaji haramu kama inavodaiwa na watu kadhaa wasioifahamu historia ya Burundi. Alidhihirisha ya kwamba, waswahili wa Burundi, haina shaka kwamba ni warundi halisi, kwa mujibu wa kisheria na hata  kihistoria. alimalizia kwa kufahamisha ya kwamba mada kama hizi zitajadiliwa mara nyingi ili kuufahamu ukweli.

Kabla ya kuufungua ukurasa wa maswali na majibu, kulitolewa kama dakika kumi hivi kwa ajili ya mapumziko madogo na ndipo watu wakapata fursa ya kuuliza maswali lukuki na kujibiwa kikamilifu. Hapa, itazingatiwa swali la aliekuwa Mkuu wa Wilaya ya Buyenzi Abdoul NZEYIMANA, aliehoji ni vipi tutajikwamua katika tatizo hili, wakati « JUWA » inajinasibu si chama cha kisiasa wakati mambo yote yaliyozungumzwa yanahusu siasa na kwamba suluhu kwa hilo ni kujiunga pekee na siasa. Pia, alifahamisha kutoelewa ni kwa nini, « ghafla », waswahili wanajikuta wakitengwa na kunyanyaswa nchini Burundi huku akionekana ni mwenye hamaki sana kwa kusema hana haja ya kujibiwa.

Lakini, Prof.Christine alishindwa kuvumilia na kutaka tu kumuweka wazi ya kwamba, tatizo la kutengwa kwa waswahili, halikuanza ghafla kama anavodai yeye bali ni la tangu kitambo ukichunguza historia pindi UNARU ilivowekwa kando kwa visingizio visivyo na msingi eti ni wahamiaji na kadhalika. Ama kuhusu jawabu la waswahili, alionyeshwa ya kwamba ingawaje « JUWA » ni chama cha Utamaduni, kitatoa mchango wake katika kupambana na hata kutetea haki za waswahili nchini Burundi huku A.MTOKA akiutoa mfano wa ‘Amnesty International’ inavojishughulisha na mengi duniani wakati si chama cha kisiasa.

Kabla ya hapo, mwandishi wa habari wa kituo cha Redio Isanganiro, Excellent NIMUBONA, alihoji swali kuhusu kuhusishwa kwa waswahili na waislamu, swala ambalo huleta utata kwa wasiolizingatia. Na ndipo akajibiwa kiuwazi kabisa ya kwamba, hata kama waswahili wengi wa Burundi ni waislamu, lakini WASWAHILI haimaanishi WAISLAMU na wala wote si waislamu, pia waislamu wote si waswahili.

Mkutano wenyewe ulimalizika vema majira ya saa mbili kasorobo usiku ambapo Sheikh Salum Issaaliwashukuru wote walioitika wito huo na haswa Prof.Christine na ndipo sote kwa pamoja tuliweza kupata fursa ya kuchangia chakula cha jioni katika hali ya utulivu na furaha. Siku iliyofuata, kuliendeshwa kongamano kama hili, ila kwa lugha ya kiswahili hapahapa mjini Brussels.

Kabla kabisa ya kufikia tamati, naomba mniruhusu wasomaji wangu wapendwa, nigusie baadhi ya yale ambayo sikupendezwa nayo. ikiwa sote ni binaadamu, hakuna aliekamilika.

Kwanza, mpaka leo hii sijaelewa kwa nini kunako mkutano huo, maadili ya kiislamu yalionekana kutengwa kabisa. Ingawaje tunafahamu, kama nilivofahamisha hapo awali, asilimia kubwa ya waswahili wa Burundi ni waislamu, kwanini Mkutano haujafunguliwa wala kumaliziwa kwa kusomwa Maneno Matukufu ya Mungu kama dini yetu inavotufunza? Wakati ambapo masheikh walikuwepo hapo na hawakuonyesha kukerwa ama kuulizia jambo hili. 

Pili, sijaridhishwa hata kidogo na idadi ya watu waliyokuwepokatika mkutano huo, licha ya njia zote zilizo tumiwa ili kuzagaza kongamano hili muhimu. Binafsi, nawalaumu waswahili wenzangu waishio Ubelgiji kwa ujumla na hususan waliopo Brussels kwa kushindwa kuhudhuria wakati idadi yao kama nnavofahamu mie, ni kubwa sana. La kushangaza na kusikitisha ni kwamba walionekana wengi mno katika sherehe za wiki moja iliyopita (SOIREE DE GALA) iliyowajumuisha wanamuziki mbalimbali hapa mjini Brussels.

Msisitizo wa lawama zangu nazitupia kwa Wanachama wa « NEW GENERATION ISHAKA », ambao, wakati wa mkutano uliofanyika Brussels tarehe 18 Februari 2012, walikubali kutoa ushirikiano katika hili ila la kushangaza hata kuhudhuria hawajaonekana. Ni jambo la kuhuzunisha sana kwa kuona jamii yetu inajali mambo ya hanasa kuliko yale yenye umuhimu zaidi. Hii itaendelea kutoa picha ya kwamba tunapenda na kujali vitu rahisi na vya burudani pekee na kamwe hatujishughulishi na kutafakari kwa kina matatizo yanayo tukabili. Tusisahau ya kwamba  » UMOJA NI NGUVU NA UTENGANO NI UDHAIFU », pia « HATUWEZI KUPATA UGALI KWA KUUPEPERUSHA UNGA ANGANI !!! »

 

Imeandikwa mjini Brussels, tarehe 21 Julai 2012 na BAKARI Ubena. >>>Haki zote zimehifadhiwa.<<<