Archive pour mai, 2015

UTAWALA WA NKURUNZIZA WAVUTIA PUMZI ZA MWISHO.

4 mai, 2015

PhotoGrid_1430771324904

 

Ikiwa imetimia siku ya saba wananchi wakiandamana nchini Burundi ili kupinga muhula wa tatu wa Nkurunziza, sasa hali inaonyesha wazi kuwa utawala huo unaelekea kufika tamati na kwa hali mbaya zaidi licha ya kutumia nguvu za dola kwa kuendesha vitisho na mauji kwa raia wasio na hatia.

Watu zaidi ya 12 wameuawa tangu kuanza kwa maandamano hayo mjini Bujumbura huku wengine wengi wakijeruhiwa na kutupwa korokoroni. Watetezi wa haki za binaadamu na wale wa mashirika ya kiraia walitishiwa na hata kukamatwa pia. Redio zilifungwa na wanahabari kunyanyaswa na kutishiwa maisha. Maelfu ya wananchi walikimbia nchi jirani. Na shughuli zote zilisimama kwa muda wote huo.

Hayo ndio matokeo ya siku za hivi karibuni nchini Burundi baada ya rais mstafu Pierre Nkurunziza kutaka kuwania tena kiti cha urais kinyume na katiba ya nchi na pia makubaliano ya Arusha. Baraza la Umoja wa Ulaya lilimtaka Nkurunziza kuachana na nia yake hiyo bila manufaa. Ban Kin Moon, Katibu wa Umoja wa Mataifa pia alimsisitizia hilo bila jibu lolote. Sasa wakati umewadia. Kila lenye mwanzo lina wake mwisho. Na huu wa Nkurunziza na genge lake utakuwa mbaya mno.

Akiwa ziarani nchini Kenya, Katibu Mkuu wa Serikali ya Marekani bwana John Kerry amesema wazi kuwa Marekani haikubaliani hata kidogo na swala hilo la Nkurunziza kuwania muhula wa tatu wa urais na kuwa nchi yake itaendelea kufuatulia kwa makini maendeleo ya alichokiita utetezi wa haki na demokrasia nchini Burundi. Hii ni wazi kuwa Marekani haitoruhusu ukiukwaji wa sheria na hasa ikizingatiwa vurugu zinazoendelea nchini Burundi kwa sasa.

Baada ya serikali ya Nkurunziza kumfuta kazi balozi wake nchini Ubelgiji, sasa ni zamu ya naibu mwenyekiti wa baraza la kulinda katiba bwana Sylvère Nimpagaritse kukimbia nchi kwa kuhofia usalama wake. Ikumbukwe kuwa baraza hilo liliombwa na baraza la seneti kujieleza kuhusu muhula huo. Sylvère alisema wazi kuwa yeye na baraza zima la kulinda katiba wanapinga vikali awamu hiyo ya tatu ya Nkurunziza na kutaja kuwa alitishiwa kuuwawa na ndio aliamua kuondoka nchini.

Tuwakumbushe kuwa baadhi ya vyombo vya habari nchini Burundi, viliandika wazi kuwa rais Nkurunziza kwa sasa atakuwa na tatizo la upungufu wa akili na ndio maana hajui akifanyacho wala muelekeo wa taifa. Na kuwa alikua akimsubiri daktari wake « psychiatre » ili amtulize kwa kumuongezea dozi ama kwa lugha nyengine « vidonge vya kupunguza kasi ya uchizi » na msongamano wa kimawazo « anti-depresseur ».

Hatimae, boti ya Nkurunziza na genge lake sasa imejaa maji na karibia itazama. Kuliko kupunguza mizigo wanapakia pia mawe. Washauri wake pia wamezidiwa na hawajui kipi wafanye. Maji yamekwisha zidi unga. Wakubali matokeo kuwa ugali hauliki tena bali uji. Na uji wataka viungo. Alamsiki.

BAKARI Ubena.