SHINIKIZO LA JUMUIYA YA KIMATAIFA KWA BURUNDI LAENDELEA.

Katika tangazo la baraza la amani na usalama la Umoja wa Mataifa la oktoba 17, walitoa wito kwa serikali ya Burundi kuanzisha mazungumzo na upinzani mjini Kampala ao Addis Abbeba, yatakaowajumuisha wahusika wote. Wito huo, uliungwa mkono na Umoja wa Ulaya, Marekani na hata Umoja wa Mataifa.

Ili kujibu wito huo,serikali ya Burundi iliteua tume ya taifa ili kuendesha mazungumzo baina ya warundi, CNDI kifupi chake kwa kifaransa na yenye muhula wa miezi 6. Mazungumzo hayo bila shaka, yatawatenga wapinzani wanaodaiwa kuwa waliendesha jaribio la mapinduzi, na ambao wanasakwa na vyombo vya sheria nchini Burundi.

Kwa upande wa serikali, wanadai kuwa, yatakuwa mazungumzo ya kitaifa baina ya warundi bila ya kuwepo upatanishi wa kimataifa. Na hivo, tume hiyo itashughulikia matatizo kadhaa yaliyotokana na uchaguzi uliopita na hata kutafutia suluhu mgogoro wa kiusalama na hata ule wa kisiasa.

Hata hivyo, tume hiyo ya CNDI bila shaka haiaminiki na haina uzito wowote mbele ya jumuiya ya kimataifa na tayari wameonyesha kuwa hiyo si suluhisho kwa mgogoro wa sasa, kwa kuwa, wanaepuka kuendesha mazungumzo ya kina na wapinzani wote.

Kwa mujibu wa taarifa kuhusu Burundi ya msemaji wa Muwakilishi na Makamo rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, iliyotolewa hii leo ijumaa, Novemba 6, Kuendelea kwa vurugu nchini Burundi ni ishara kuwa mgogoro wa sasa unapevuka.

Kauli za hivi karibuni za viongozi wa serikali zinaweza kuchochea hali ya sasa na ndio maana Umoja wa Ulaya unawatolea wito wadau wote kujizuia na kuheshimu majukumu yao. Kuchochea ghasia na mgawanyiko ni tishio kubwa na la ziada kwa usalama na utulivu wa nchi ya Burundi.

Umoja wa Ulaya umeendelea kuwaonya viongozi wa serikali kushiriki katika mashauriano chini ya ibara ya 96 ya Mkataba wa Cotonou ili kupatia ufumbuzi utakaokubalika na pande zote ili kukomesha ukiukwaji wa vipengee muhimu vya haki za Binaadamu ambazo ni kanuni za kidemokrasia na utawala bora.

Mashauriano hayo ambayo yataendeshwa kwa nia ya majadiliano na ushirikiano, yatakua pia na lengo kuu la kuunga mkono juhudi za kuhakikisha amani ya kudumu nchini Burundi.

Umoja wa ulaya umepongeza na kuunga mkono kauli ya mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika ya novemba 4, na kutaja kuwa itatoa msaada wake kunako juhudi za upatanishi wa Uganda na hata ule wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki.

Hatimae, umoja wa ulaya kupitia muwakilishi wake mkuu, wanataraji kuwa Serikali ya Burundi itatumia kila liwezekanalo ili kuanzisha mazungumzo ya kitaifa kwa kuheshimisha mkataba wa amani wa Arusha.

BAKARI Ubena

Laisser un commentaire