BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA LAPASISHA AZIMIO LA UFARANSA KUHUSU BURUNDI.

umojaHofu ya Jumuiya ya Kimataifa ni kuona Burundi ikikumbwa na machafuko makali. Ndio maana hii leo jioni, Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lilikutana ili kupiga kura juu ya pendekezo la Ufaransa lenye dhamira ya kuwawekea vikwazo wale wote wanaochochea vurugu na hata kulazimu mazungumzo kati ya wadau wote nchini Burundi ili hatimae kupata suluhu ya kudumu na itakayokubaliwa na pande zote.

Hii leo alkhamisi ya Novemba 12 mwaka 2015, Umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, wametoa tangazo la pamoja linalowataka serikali na Upinzani kukutana haraka sana ili kusitisha vurugu na kupatishia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa sasa.

Viongozi waandamizi wa jumuiya hizo, walitoa wito huo huko visiwani Malta walipokutana ili kujadili mfumo wa kuhimili wimbi la wakimbizi kutoka Afrika na wanaoelekea barani Ulaya na hivo kusababisha vifo vya mamia ya watu wanaokufa maji wakijaribu kuvuka na kuingia kwenye ardhi ya ulaya.

Msimamo ni ule ule, mazungumzo hayo ni lazima yaendeshwe mjini Kampala Uganda ama Addis Abeba, Ethiopia na yasimamiwe na Yoweri Museveni, msuluhishi alieteuliwa na Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki tangu mwezi Julai mwaka huu.

Katika zoezi hilo la kura hii leo katika baraza la usalama la umoja wa mataifa, kuna uwezekano, endapo serikali itaendelea kukaidi, kutumwa kwa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa na hata vile vya umoja wa afrika. Hata hivyo, Katibu mkuu wa umoja wa mataifa anazo wiki 2 ili kusahihisha hilo.

Kwa mujibu wa kifungo nambari 7 , umoja wa mataifa unaruhusiwa kutumia nguvu ili kurejesha amani. Hilo ni lazima liafikiwe na tume maalum ya umoja wa mataifa ama likubaliwe na nchi husika.  Tayari kwa pamoja, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha Azimio lilotolewa na Ufaransa.

Wengi walikuwa wakihofia uzito wa kufaanikisha hili, kutokana na Urusi, ambayo ina kura ya turufu yaani « droit de Veto » katika baraza hilo la umoja wa mataifa, kupinga vikali kwa muda kadhaa azimio hilo na kutaja kuwa, hayo ni matatizo ya ndani ya Burundi yanayotakiwa kusuluhishwa na warundi wenyewe. Hata hivyo, katika kura ya hii leo, NCHI ZOTE ZIMEAFIKI AZIMIO HILO.Hata hivyo, serikali ya Bujumbura, kupitia mshauri wa rais anaehusika na mawasiliano, Willy Nyamitwe, imekwishataja wazi kuwa inapinga vikali azimio hilo na kutaja kuwa kamwe hawawezi kulazimishwa sehemu inayotakiwa kuendeshwa mkutano huo.
Baadhi ya wanadiplomasia wanahofia pia uingiliaji kati wa rais Paul Kagame wa Rwanda, baada ya kuwatuhumu viongozi wa Burundi kuwa wanawaua kiholela raia wao usiku na mchana. Uhusiano baina ya nchi mbili hizo jirani ni mbaya mno na wote wanatupiana lawama na tuhma mbalimbali.

Bila shaka kuna hatari ya kuzuka machafuko mabaya nchini Burundi, lakini mpaka muda huu, hakuna sababu zozote zinazoweza kubaini kuwa, kuna mpango wa mauaji ya kimbari unaowavizia watutsi pekee. Jambo la muhimu, ni kuepuka kukuwa kwa vurugu na mauaji na wadau wote wakubaliane ili hatimae mgogoro huu umalizike.

Marekani nayo inaendelea kuvalia njuga tatizo la Burundi. Baada ya Mjumbe wa Rais Obama kumaliza ziara yake ya siku mbili mjini Bujumbura, sasa, Bwana Thomas Perriello amejielekeza nchini Uganda ili kuzungumza na rais wa nchi hiyo, na kumtaka aitishe mkutano wa haraka baina ya serikali na Upinzani.

Pia, Rais wa Marekani mwenyewe aliongea kwa simu na yule wa Afrika ya Kusini. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, hiyo jana, rais wa marekani Barack Obama, aliongea kwa njia ya simu na rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma ili kumuelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Burundi.

Rais Obama amemuomba Rais Zuma kuendelea kushirikiana na watendaji wengine wa kikanda ili kutoa wito wa utulivu na kuhamasisha mjadala ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro wa sasa.

Watu zaidi ya 200 wameuwawa na wengile laki mbili kuihama nchi tangu mwezi April, pale Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kugombea muhula wa tatu ambao kwa mujibu wa wapinzani, unakiuka katiba na mkataba wa Arusha.

Jumuiya ya kimataifa inahofia kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kama hapo awali, vilivyosababisha vifo vya watu laki tatu.

BAKARI Ubena

Laisser un commentaire