KWAHERI 2014, KARIBU 2015.

22 décembre, 2014

bandeau-annee-2015.jpg

Naomba nitangulize salamu zangu za dhati kwenu nyote. Ni matumaini yangu kuwa mpo wazima wa afya na kwamba mwaka 2014 ambao kwa uwezo wake Mola tunatarajia kuumaliza, ulikuwa wenye kheri na fanaka.        Sina budi kuwatakia kheri zaidi kwa mwaka ujao wa 2015. Niwatake pia radhi kwa ukimya wa muda mrefu.

Dhamira ya kurudi hewani ni kutaka tujuzane na kujadili mada mbalimbali zinazohusu nchi yetu ya Burundi.     Ila kwa leo, ni haswa kukujulisheni ujio wangu tena hewani ili kupambanua yaliyoficwa na kuelezea yote hayo kinaga ubaga. Pia, tutakuwa tunakufikishieni yanayojiri barani ulaya katika jamii yetu ya Warundi.

Lakini kabla hatujaagana kwa siku ya leo, hebu tujadili mawili matatu kuhusu serikali ya Bwana NKURUNZIZA ambayo inatuongoza. Mwaka 2014 ndo huo unatokomea, ni yapi kwa ujumla serikali hii imeyatenda ili kuendeleza nchi yetu?

Binafsi naona kama tumejishughulisha mno na maswala yasio maana kuliko yale yenye umuhimu zaidi kwa taifa letu. Ikiwa raia, mashirika ya kibinafsi na ya kutetea haki mbalimbali, Viongozi tawala na hata wale wa upinzani, sote tumo katika kapu moja. Viongozi tawala huficha ukweli kwa wananchi na wananchi wala hawaulizii kuhusu hilo. Nao viongozi wa vyama vya upinzani wamepumbazika na kuyataka madaraka. Miongoni mwa tuliyosahau kujishughulisha kwayo ni pamoja na:

1. UCHUMI WA TAIFA.

Licha ya kuzungumzia swala hili juu juu, sijawahi kuskia wala kuona yeyote akijishughulisha na swala hili ama kufanya mijadala na kuandaa makongamano ili kuzungumzia swala hili kwa undani zaidi kama inavofanyika katika nchi kadha zenye maendeleo, mfano barani ulaya. Raia pia wanayo haki ya kujua uchumi wa nchi yao umefkia wapi, watachangia kiasi gani na kwa namna ipi na si kupandisha bei za bidhaa  na kuongeza kodi na ushuru kiholela.Mfano ni nani ajuae deni la serikali kwa sasa? Ao kiwango gani kipo tayari kwa mipango ya serikali, na ngapi zinahitajika ili kupata usawa wa bajeti ya mwaka huu na ujao?

2. PROGRAMU YA SERIKALI.

Kabla ya kuongoza, serikali nzima kwa ujumla lazima iwe na programu maalum itakayofuatishwa kwa muhula wote wa uongozi hususan kila waziri huandaa programu yake ili kuonyesha kipi anatarajia kukifanya, kukiboresha katika uongozi wake. Programu hiyo, lazima iwe wazi na gharama zake kufahamika ili kuepukana na vitendo kadha vya utumiaji mbaya wa mali ya umma. Hili ni jukumu la serikali kwa raia wake.

Hivi nani ajuae programu ya serikali yetu kwa sasa, hata kwa mwaka 2014 tuu, na kiasi gani cha pesa kimetumika na kwa miradi gani. Ndio maana tusishangae rushwa kuongezeka nchi mwetu, huku viongozi wakigawana madaraka ili kila mmoja apate kumega tonge lake na kuwaacha raia patupu wakiteseka na kukosa la kufanya.
3.MIZANIA (BILAN)

Imezoeleka ya kwamba, serikali inapomaliza mwaka, kufanya mizania ya uongozi wake ili kujua ni yapi wameyatekeleza, ambayo hayajakamilika na wanayotarajia kuyafanya. Nasisitiza tena kuwa, yote haya, baada ya uchunguzi na utendaji kazi, raia wanatakiwa kujulishwa ili wajua maendeleo ya nchi yao.  Haya ni mojawapo mwa mengi ambayo tumeyasahau. Tuache kushughulika na tuyaonayo tu, tujibanze na mengine pia.

Hatimae, ningependa pia kutoa ushauri kwa viongozi wetu wa sasa, kumbukeni kuwa hapo mlipo kuna walio watangulieni na kamwe hamtokaa milele maana cheo ni dhamana, na ni koti tuu, leo mmelivaa na ipo siku mtalivua. Je, koti hilo mtalirusha katika hali gani? Matendo yenu ipo siku yatawekwa wazi na kuhukumiwa. Fanyeni yaliyo mema kwa raia wenu, bado hamjachelewa. Hakuna binaadamu aliekamilika. Na kwa wale wapinzani, msiwe tu wenye kupiga kelele na kuyaonyesha mabaya tu bila ya kutoa pendekezo lolote ili kuboresha na kuimarisha hali flani. Sina budi kutia nanga kwa leo, nikiwatakia kwa mara nyingine sikukuu njema.

BAKARI Ubena

Haki zote zimehifadhiwa/BD/Disemba 2014

 

 

 

KONGAMANO LA KWANZA LA KIHISTORIA KWA WASWAHILI WA BURUNDI.

23 juillet, 2012

KONGAMANO LA KWANZA LA KIHISTORIA KWA WASWAHILI WA BURUNDI. dans Liens conferHabari wasomaji wangu wapendwa. Ni furaha isiyo kifani kukutana nanyi tena kunako safu hii. Nimshukuru Mola kwa kuendelea kuniazima pumzi na afya njema hadi kufkia utekelezaji wa hili na mengineyo mengi yanayogubika maisha yangu ya kila siku, pia nizidi kumshukuru kwa Kuendelea kunijaalia mema na kuniepusha na mabalaa. Kwa niaba yenu sote, namuomba Atusamehe, Atuongoze na Atupe mwisho uliyo mwema. (Amin).

Kwa mara ya kwanza kabisa, kulihudhuriwa kongamano la kwanza kabisa na ambalo ni la kihistoria kwa waswahili wa Burundi. Kongamano hilo liliendeshwa mjini Brussels Ijumaa ya tarehe 13 Julai 2012, kwa kuandaliwa na Jumuiya ya Waswahili  » JUWA », shirikisho la kitamaduni. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi mdogo upatikanao Schaerbeek (Place de la Reine 12).

Licha ya kuanza kwa kuchelewa takriban dakika thelathini (30) ili kuendelea kuwasubiri washiriki wa kongamano lenyewe, bado idadi ya watu waliohudhuria ilikuwa si ya kuridhisha mno hadi kudhihirika kuwa asilimia kubwa ya viti kubaki vitupu. Ila binafsi, hilo si tatizo, maana, bora jiwe la dhahabu kuliko mlima wa tope.

Mkutano ulifunguliwa kwa riwaya ndogo ya Sheikh Salum Issa kwa utangulizi na kumpa fursa Ahmadi Kassa kuanza rasmi kuelezea sababu na umuhimu wa kongamano lenyewe na kufahamisha kuwa Ubelgiji imechaguliwa kuupokea mkutano huo wa kwanza kutokana na sababu kadhaa za kihistoria.

A.Kassa alifahamisha ya kwamba, haitoshi kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Burundi kwa sherehe pekee bali pia kutumia fursa hiyo kuyatafakari mengi baina ya maswali yanayoikabili jamii yetu, kama vile kuifahamu historia ya waswahili wa Burundi na ni upi mchango wa waswahili katika kugombea uhuru wa nchi hiyo.

Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya Mwanahistoria na Professa Christine DESLAURIER, ambae pia alikuwa mgeni rasmi, kuyaweka bayana maswali hayo ambapo aliyafafanua kwa takriban masaa mawili huku watu wakionekana kunogewa na kutaka asimalize kuongea. Lakini, kabla kabisa hajaanza kusimulia historia hiyo tamu, alifahamisha ya kwamba kuna uwezekano kwa anaehitaji kupata historia zaidi ya Burundi kabla na baada ya Uhuru, kuzitembelea Ofisi za Idara ya « Kumbukumbu » za Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji zipatikanazo mjini brussels. Kwa kuwa, baada ya miaka 50, sheria zimebadilika na kuna nyaraka ambazo zimewekwa wazi kwa wasomaji tofauti na hapo awali.

Hapo alisisitizia kuhusu waraka nambari { BUR ,64} katika kumbukumbu, unaoweka wazi ya kwamba, si pekee chama UPRONA kilichosimama kidete kwa kupigania UHURU wa BURUNDI, bali hata kabla yake kulikuwepo chama UNARU pia hata na raia kadhaa wazalendo waliojaribu kusitisha Ukoloni kwa njia moja ama nyengine. Mfano wao ni INAMUJANDI alieitwa mchawi kwa kupambana moja kwa moja na wawakilishi wa wakoloni. WAKULIMA ambao walitumia mfumo wa kukojolea mimea ya kahawa waliopanda ili kuhujumu amri za ukoloni, na kadhalika.

Baaada ya kufahamisha ni jinsi gani shirika-chati za Ukoloni zilivokuwa, bi Christine aligusia swala nyeti na kuonyesha ni kwa nini WASWAHILI walinyanyaswa na hata kutengwa na Wakoloni wa Ubelgiji ili wasipate elimu na mengineyo. Sababu kuu ilikuwa ni kutokana na dini yao. Ikiwa Ukoloni ni wa Kikristo na asilimia kubwa ya waswahili ni waislamu, basi wakoloni hao walifanya kila njama ili kuhujumu jamii ya waswahi na hata wa protestanti. Katika kipindi hicho, Buyenzi ilikuwa na idadi ya raia elfu kumi (10.000) na kwa mujibu wa wakoloni, pasenti sitini (60%) ni wakongomani, pasenti thelathini (30%) warundi na pasenti zengine nane (8%) ni wanyarwanda, wakati ambapo raia wote hao, kwa ukweli na kisheria walikuwa ni warundi. Inafahamika wazi ya kwamba, raia hao walikuwa na uhusiano wa karibu na Tanganyika ( ambayo ni Tanzania kwa sasa). Na waswahili wengi walipatikana katika maeneo ya BUYENZI, BWIZA, RUMONGE, NYANZA-LAC na KITEGA (kwa sasa GITEGA).

Kutokana na utafiti mpana na kwa mtazamo wake, Professa Christine anamnadi « SALUM HASSAN MASHANGWA » kama shujaa wa utetezi wa Uhuru wa Burundi, kuanzia miaka ya 1956. Licha ya kuwa na chimbuko la Tanganyika, alikuwa mtu muhimu katika chama UNARU, pia mfadhili. Alimiliki magari kadhaa, alifaanikiwa kuunda Ofisi binafsi ya Uchapishaji (MURASABE, UHURU na UMOJA) ambazo zilikuwa zikizagazwa kwa siri, kwa kuhofia wakoloni. Pia, mnamo miaka hiyohiyo ya 1956, aliunda chama cha kitamaduni « BARAFU NYEUPE », ambacho kiliwakusanya asilimia kubwa ya akina mama na yeye kushikilia nyadhifa ya Katibu mkuu, kwa kuwa kipindi hicho, ilikuwa hairuhusiwi kuunda chama cha kisiasa. S.H.MASHANGWA, alitumia ujanja kwa kuwasajili akina mama wengi katika chama chake, ili waweze kuzagaza nakala zake hadi Tanganyika, kwa kuwa wao walikuwa hawatiliwi sana mashaka wala kukaguliwa sana mipakani tofauti na wanamume.

Pia, mnanzoni mwa mwaka 1958, MASHANGWA akishirikiana na wengine kama akina BICHUKA, walimuunganisha Mwanamfalme Louis RWAGASORE na Rais wa TANGANYIKA, J.K. NYERERE, alipotuwa kwa muda mjini USUMBURA akielekea GHANA katika Mkutano mkuu wa ACCRA wa march 1958). Ni baada ya hapo, mnamo mwaka 1959, ndipo kukaruhusiwa uundwaji wa vyama vya kisiasa na moja kwa moja kukaundwa chama UNARU, baadae UPRONA na vinginevyo. Mwanzoni, licha ya kuwa na upinzani mdogo, vyama hivyo viwili, vilikuwa na dhamira moja, ambayo ni kugombea UHURU WA BURUNDI.

Waliyohudhuria kongamano hilo, watakubaliana nami ya kuwa, historia hiyo ya kabla, wakati na baada ya uhuru, ni ndefu mno, kama alivotaja mwenyewe Prof.Christine. Picha za sanamu (video) zilizochukuliwa siku hiyo pia na usomaji wa vitabu, ndio utawasaidia kuyafahamu mengi zaidi. Binafsi, nilifurahishwa na alivodadisi swala nzima la kihistoria na kuonyesha umuhimu wa waswahili katika kupambana na kupigania uhuru wa Burundi.

Kabla ya kumalizika kongamano hilo, alipewa nafasi mwanaharakati mkubwa wa swala zima la waswahili wa Burundi, Abdoul MTOKA ambae pia ni mwanasheria, aliefafanua kwa mukhtasari sababuza kupigania Uhuru na kusisitiza kuhusu Unyanyasaji waliofanyiwa waswahili nchini Burundi, hali ambayo bado inaendelea hadi sasa. aliweka wazi kwamba, watu huwa hawagombei uhuru ili wasitishe pekee ukoloni, bali pia waweze kupata mafaanikio ya uhuru wao ambayo yalikuwa yakizuiliwa na Ukoloni.

Na moja wapo mwa hayo ni: – Kutengwa katika utapataji wa elimu

- Kulazimishwa kulipa kodi na ushuru vya hali ya juu

- Kufurushwa kinyume cha sheria katika makaazi yao  (ardhi zao) bila ya kupewa viinua mgongo, nk.

Na hadi sasa, twaadhimisha miaka 50 ya Uhuru, na nina imani kwamba bado kuna unyanyasaji kwa waswahili wa Burundi na kazi kubwa bado inahitajika kufanyika ili kufikia malengo thabiti. Pia, A.MTOKA, aligusia kuhusu historia ya waswahili ili kuonyesha wazi kwamba si wageni la wahamiaji haramu kama inavodaiwa na watu kadhaa wasioifahamu historia ya Burundi. Alidhihirisha ya kwamba, waswahili wa Burundi, haina shaka kwamba ni warundi halisi, kwa mujibu wa kisheria na hata  kihistoria. alimalizia kwa kufahamisha ya kwamba mada kama hizi zitajadiliwa mara nyingi ili kuufahamu ukweli.

Kabla ya kuufungua ukurasa wa maswali na majibu, kulitolewa kama dakika kumi hivi kwa ajili ya mapumziko madogo na ndipo watu wakapata fursa ya kuuliza maswali lukuki na kujibiwa kikamilifu. Hapa, itazingatiwa swali la aliekuwa Mkuu wa Wilaya ya Buyenzi Abdoul NZEYIMANA, aliehoji ni vipi tutajikwamua katika tatizo hili, wakati « JUWA » inajinasibu si chama cha kisiasa wakati mambo yote yaliyozungumzwa yanahusu siasa na kwamba suluhu kwa hilo ni kujiunga pekee na siasa. Pia, alifahamisha kutoelewa ni kwa nini, « ghafla », waswahili wanajikuta wakitengwa na kunyanyaswa nchini Burundi huku akionekana ni mwenye hamaki sana kwa kusema hana haja ya kujibiwa.

Lakini, Prof.Christine alishindwa kuvumilia na kutaka tu kumuweka wazi ya kwamba, tatizo la kutengwa kwa waswahili, halikuanza ghafla kama anavodai yeye bali ni la tangu kitambo ukichunguza historia pindi UNARU ilivowekwa kando kwa visingizio visivyo na msingi eti ni wahamiaji na kadhalika. Ama kuhusu jawabu la waswahili, alionyeshwa ya kwamba ingawaje « JUWA » ni chama cha Utamaduni, kitatoa mchango wake katika kupambana na hata kutetea haki za waswahili nchini Burundi huku A.MTOKA akiutoa mfano wa ‘Amnesty International’ inavojishughulisha na mengi duniani wakati si chama cha kisiasa.

Kabla ya hapo, mwandishi wa habari wa kituo cha Redio Isanganiro, Excellent NIMUBONA, alihoji swali kuhusu kuhusishwa kwa waswahili na waislamu, swala ambalo huleta utata kwa wasiolizingatia. Na ndipo akajibiwa kiuwazi kabisa ya kwamba, hata kama waswahili wengi wa Burundi ni waislamu, lakini WASWAHILI haimaanishi WAISLAMU na wala wote si waislamu, pia waislamu wote si waswahili.

Mkutano wenyewe ulimalizika vema majira ya saa mbili kasorobo usiku ambapo Sheikh Salum Issaaliwashukuru wote walioitika wito huo na haswa Prof.Christine na ndipo sote kwa pamoja tuliweza kupata fursa ya kuchangia chakula cha jioni katika hali ya utulivu na furaha. Siku iliyofuata, kuliendeshwa kongamano kama hili, ila kwa lugha ya kiswahili hapahapa mjini Brussels.

Kabla kabisa ya kufikia tamati, naomba mniruhusu wasomaji wangu wapendwa, nigusie baadhi ya yale ambayo sikupendezwa nayo. ikiwa sote ni binaadamu, hakuna aliekamilika.

Kwanza, mpaka leo hii sijaelewa kwa nini kunako mkutano huo, maadili ya kiislamu yalionekana kutengwa kabisa. Ingawaje tunafahamu, kama nilivofahamisha hapo awali, asilimia kubwa ya waswahili wa Burundi ni waislamu, kwanini Mkutano haujafunguliwa wala kumaliziwa kwa kusomwa Maneno Matukufu ya Mungu kama dini yetu inavotufunza? Wakati ambapo masheikh walikuwepo hapo na hawakuonyesha kukerwa ama kuulizia jambo hili. 

Pili, sijaridhishwa hata kidogo na idadi ya watu waliyokuwepokatika mkutano huo, licha ya njia zote zilizo tumiwa ili kuzagaza kongamano hili muhimu. Binafsi, nawalaumu waswahili wenzangu waishio Ubelgiji kwa ujumla na hususan waliopo Brussels kwa kushindwa kuhudhuria wakati idadi yao kama nnavofahamu mie, ni kubwa sana. La kushangaza na kusikitisha ni kwamba walionekana wengi mno katika sherehe za wiki moja iliyopita (SOIREE DE GALA) iliyowajumuisha wanamuziki mbalimbali hapa mjini Brussels.

Msisitizo wa lawama zangu nazitupia kwa Wanachama wa « NEW GENERATION ISHAKA », ambao, wakati wa mkutano uliofanyika Brussels tarehe 18 Februari 2012, walikubali kutoa ushirikiano katika hili ila la kushangaza hata kuhudhuria hawajaonekana. Ni jambo la kuhuzunisha sana kwa kuona jamii yetu inajali mambo ya hanasa kuliko yale yenye umuhimu zaidi. Hii itaendelea kutoa picha ya kwamba tunapenda na kujali vitu rahisi na vya burudani pekee na kamwe hatujishughulishi na kutafakari kwa kina matatizo yanayo tukabili. Tusisahau ya kwamba  » UMOJA NI NGUVU NA UTENGANO NI UDHAIFU », pia « HATUWEZI KUPATA UGALI KWA KUUPEPERUSHA UNGA ANGANI !!! »

 

Imeandikwa mjini Brussels, tarehe 21 Julai 2012 na BAKARI Ubena. >>>Haki zote zimehifadhiwa.<<<

 

 

 

 

 

 

MIAKA 50 YA UHURU WA BURUNDI .

14 juin, 2012

Hymne national du Burundi sur \ »Youtube\ » MIAKA  50 YA UHURU WA BURUNDI . dans Liens bdi-flag

Nitangulize salamu zangu za dhati kwa wasomaji wangu wapendwa, pia nikichukua fursa hii kukutakeni radhi kutokana na ukimya wa muda kadhaa bila ya kukutana nanyi kunako makala kama hizi.

Hakika, kila sifa njema anastahili apewe Mola wa viumbe wote, alieweza kuumba usiku na mchana, akaumba ardhi na mbingu bila ya kuweka nguzo. Tumuombe Maanani atuongoze tuwe miongoni mwa waja wake wema, atupatie maisha marefu yenye furaha, usalama na amani hapa duniani mpaka huko mbinguni.

Atuongoze pia tuwe ni wenye kumkumbuka kila wakati, atuwezeshe kuishi kwa kupendana na kuhurumiana, tuachane na kufanyiana hiyana na atufanye ni wenye kusaidizana. Pia, asituweke kuwa ni wenye huzuni wakati wote na atuondolee shida zetu za utafutaji wa riziki zinazotutesa kila wakati. (Amin)-

Kama kinavoashiria kichwa cha habari, nchi yetu Burundi inajiandaa July mosi mwaka huu wa 2012, kusherehekea sikukuu ya miaka 50 ya Uhuru wake kutoka kwa wakoloni « Ubelgiji ».

Wengi miongi mwetu, tunaiona siku hiyo ya kipekee kama tuu sherehe ambapo wafanyakazi na wanafunzi, jeshi na polisi hufanya gwaride mbele ya rais wa jamhuri huku harakati mbali mbali za kunogesha sherehe hiyo zikiendelea kutuburudisha.

Sintothubutu kuwalaumu wenzangu wanaofanya hivo, lakini binafsi, huwa napendelea kusherehekea kitu ambacho kwa dhati moyoni kinanifurahisha ao japo kinachonipa sababu kadhaa za kufanya hivo. Hapa, nang’amua kwamba, ni busara zaidi kutatmini kwa makini ni yapi mafaanikio ambayo nchi yetu imeyafikia katika kipindi chote hicho cha miaka 50 hadi sasa.

Sintoweza kuchambua vipengee vyote muhimu ambayo nchi yoyote duniani huwa inajaribu kuviboresha ili kujiona kufikia maendeleo inayotarajia. Hebu nijikite kwa mambo mawili tu (2) muhimu ambayo Burundi inahitaji kuendeleza kujiimarisha zaidi.

  1. KUSIKILIZANA na KUVUMILIANA KATIKA HOJA:

Sote tunafahamu kuwa nchi yetu imekwisha kumbwa kwa maraa kadha na machafuko mengi na yenye sababu mbalimbali ambazo sintopendelea kukumbushia kwa leo. Na hii hutokana haswa na tatizo la kutokuwa na ukomavu wa kisiasa kwa kutosikilizana na kuvumiliana katika hoja.

Sifa moja kubwa ya mwanademokrasia popote duniani, ni kukubali kusikiliza mawazo tofauti na yale aliyonayo yeye. Kinyume na hapo, mtu huyo huchukuliwa kama ‘dikteta’.

Unapotoa fursa ua kusikiliza, bila shaka utakuwa na nafasi ya kuyatafakari na kuyachuja mawazo ya mwenzio, lakini ukikataa kutoa fursa ya kusikiliza basi utaendelea kuwa na mawazo ya aina moja tuu. Yaani yale yanakufurahisha na ambayo kwa vyovyote yatakuwa hayajengi zaidi ya kubomoa.

Kwa hili pekee, serikali yetu ya sasa inayoongozwa na rais Pierre NKURUNZIZA, ina sifa mbaya mno hadi kimataifa inatambulika. Huwa hawatoi fursa kwa mtu mwengine alie na mawazo tofauti na ya kwao, kujenga hoja yake, kwao mtu huyo ni adui mkubwa na anaweza kujikuta katika mazingira ya hatari sana.

Ni mara ngapi watu wamefungwa bila hatia, wengine kuendeshea vipigo na mateso ya kinyama, wengine kulazimika kuihama nchi yao na baadhi kulazimika kukaa kimya kwa hofu ya uhai wao.

Watetezi wa haki za binaadamu, wanahabari, wanasiasa wa upinzani, raia wa kawaida, wanaendelea kuyapata matatizo makubwa nchini Burundi kutokana tuu na fikra ao hoja yao (japo nzuri kiasi gani) ambayo ipo kinyume na serikali ya sasa.

Kukubali kusikiliza hoja ya mwengine, haimaanishi kukubaliana na kile unachokisikiliza, lakini ile tuu kutoa fursa ya kusikiliza mawazo tofauti kunaweza kutoa fursa kwako kutumia hoja zilezile alizokuwa akizitoa yule ulieamua kumsikiliza na kujenga hoja mpya na hatimae kumuaminisha mtu yule.

Ni jambo la kusikitisha mno kwa wanasiasa wa Burundi kuwa na moyo mdogo sana wa kuvumilia mawazo tofauti na ya kwao na kukosa sifa hii ya kuwa wanademokrasia. Na hili halijaanza katika awamu hii ya Cndd Fdd, bali ni tangu kitambo, na kama nilivofahamisha hapo mwanzoni, ndio kiini cha mapigano yaliyotokea na yatakayoweza kutokea (Mola atuepushe kwayo) iwapo hili halitozingatiwa.

Ni jambo la kawaida watu kutofautiana kimtazamo na kimawazo, kwa kuwa si rahisi warundi wote, hasa wa karne hii, sote tukawa wafuasi wa chama fulani cha siasa hata kama kingelikuwa kimoja, lazima wengine watakuwa na mawazo mbadala. Hii ni kwa kuwa kila mtu anayo haki ya kuamini katika kile anachopendezwa nachona hapaswikuhukumiwa ama kuonekana ni msaliti kwa kuwa tu haungani au hakubaliani na kile kinachoaminiwa na kundi lingine la watu.

Na hili linapaswa kuwapo hata kwa viongozi na wasio viongozi. Wajue kuwa mawazo yao sio sahihi daima na anapotokea mtu akawakosoa, basi wawe tayari kusikiliza na kujirekebisha kama watagundua uzito wa hoja itakayotolewa.

Kwa kufanya hivi, tutafikia jambo hili jema na kuamini kwamba: ‘SIASA SAFI NI ILE AMBAYO VIONGOZI WANAKUBALI KUKOSOLEWA’ pale wanapokwenda tofauti na matarajio ya wengi na hapo bila shaka nchi yetu itakaa katika amani na utulivu wa kudumu, ambayo ni dhamira ya kila mwananchi alie ndani ao nje ya Burundi.

  1. BURUNDI, NCHI ‘OMBA OMBA’ DUNIANI:

Ni wazi kwamba Burundi ni miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kwa kupewa misaada kutoka wahisani mbalimbali. Wahisani wakubwa kwa mipango ya maendeleo kwa nchi yetu ni Umoja wa Ulaya, Benki ya maendeleo ya afrika, Benki ya dunia na shirika la fedha duniani.

Cha kushangaza ni kuwa kulikoni Burundi imepokea misaada mingi kiasi hichotangu ipate Uhuru, lakini imebaki kuwa moja kati ya nchi ambazo wananchi wake wanaogelea katika umaskini wa kutisha, kiasi cha wengi kuishi chini ya dola moja kwa siku.

Jibu kwa mshangao huo ni kwamba, nchi haiwezi kusonga mbele kimaendeleo kutokana na utegemezi mkubwa wa misaada hiyo ya wahisani na haswa matumizi yake mabaya ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa Utawala Bora ambapo asilimia kubwa ya misaada hiyo ikimezwa na vitendo vya rushwa. Mfano hai na wa hivi karibuni, kesi inayoshakiwa kuwa ya rushwa inayoendelea nchini Ubelgiji ambayo mhusika mkuu ni Ombusman wa Burundi, Muhamed RUKARA. Mtu ambae angetakiwa kuwa msuluhishi wa taifa na mwenye kutoa mfano mwema.

Ni aibu iliyo je kwa viongozi wetu kuwa na tabia chafu kama hizi kwa kukosa uzalendo na hata chembe ya huruma kwa kiwango kikubwa cha wananchi ambao wanaendelea kuishi maisha duni kwa ukosefu wa nyanja bora za elimu, uhaba wa miundombinu (hospitali, barabara,makaazi,katika kilimo,…), afya bora, maji safi, na kadhalika.

Sote kwa pamoja, tunapaswa kuamka na kushikamana kwa kuilazimisha serikali kuwashtaki watuhumiwa wote wa kashfa za rushwa, na adhabu kali zitolewe kwa watakaobainika kisheria. La sivyo, watazidi kunufaika watu wachache na nchi kuendelea kuwa maskini.

Kiongozi mwema ni yule ambae anae wajali wale anaowaongoza, kwa kufanya kila aliwezalo waishi katika hali ya utulivu wa nafsi, haswa kwa kuweza kukidhi mahitaji yao muhimu ya kila siku. Nayo ni kupata chakula, mavazi na makaazi. Pia, kuboresha maisha yao katika mambo mengine yeliyo muhimu kama usalama, elimu, afya, michezo na kadhalika.

Si maanishi kuwa, ni jambo rahisi ama liwezalo kutekelezwa kwa muda mfinyu, lakini endapo tukiwa na uzalendo wa kutosha, kwa kutumia ipasavyo pesa ya wananchi kwa ajili yao, hilo linawezekana. Tusisahau kuwa « Penye nia kuna njia ».

Hatimae, tuwa WAZALENDO, WAVUMILIVU na haswa WAKOMAVU katika dhamira ya kuiendeleza nchi yetu. Kwa kuwa hata siku moja, haki ya mtu huwa haipotei bali hucheleweshwa tuu. Na mafaanikio siku zote hutokana na kuwa na uvumilivu na subira hata kama unaona kitu chako si kizuri, huna sababu ya kukitupa. Unachopaswa ni kuangalia namna ya kukiboresha ili kipendeze.

BURUNDI, nchi yetu ya « maziwa na asali », daima tutakulinda na kukupenda!

« Haki zote zimehifadhiwa »

Imeandikwa mjini Brussels, Juni 14, 2012

na : BAKARI Ubena.-

 » Salaamu zangu za dhati kwa warundi wenzagu popote walipo bila ya kuwasahau wagonjwa wote, wafungwa ( haswa kwa mwanahabari mwenza: Hassan RUVAKUKI, mwanasiasa: El Hadj Hussein Radjabu), marais wote walioiongoza nchi yetu, na hata wa sasa Pierre Nkurunziza, nikiwaombea wepesi katika majukumu hayo makubwa.  »

1234